NEW UPDATES

Ataka tanesco iokolewe, iko hoi.

Makao  makuu ya tanesco jijini Dar es salaam.
JUHUDI za makusudi zinatakiwa kufanyika ili kulinusuru Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) ambalo lipo hoi kutokana na malimbikizo makubwa ya madeni.
Malimbikizo hayo yanatokana na shirika hilo,kununua umeme kwa bei ya juu kutoka kwa watengenezaji huru wa nishati hiyo (IPPs) na watengenezaji wa dharura wa nishati hiyo (EPPs).
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyowasilisha akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma jana, alisema kwamba lazima juhudi za makusudi zifanyike kuinusuru Tanesco.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad alisema juhudi zinatakiwa kuliokoa shirika katika hali lililopo kwa kutafuta vyanzo vya umeme vyenye bei nafuu.
“Jitihada zaidi zinahitajika kuliokoa shirika katika hali liliyopo kwa kutafuta vyanzo mbalada vya umeme vyenye bei nafuu,” alisema. “Tanesco inapata hasara ya Sh 265.3 kutokana na kununua umeme kwa bei ya wastani wa Sh 544.65 kutoka kwa IPPs/EPPs na kuuza kwa wastani wa Sh 279.35 kwa uniti,” aliongeza.
Profesa Assad alisema kutokana kupata hasara hiyo, shirika limeendelea kuwa katika hali mbaya na kujiendesha kwa hasara, njia pekee ya kulinusuru ni kuzalisha umeme unaotokana na maji na gesi na kuachana na wazalishaji binafsi wanaotumia mafuta.
Aliishauri serikali kutafuta fedha na kuwekeza kwenye miradi ya maji ambayo itazalisha umeme wenye bei nafuu zaidi ukilinganishwa na umeme unaotumiwa baada ya kuzalishwa na kampuni binafsi.
Alisema miongoni mwa miradi inayoweza kusaidia kuzalisha umeme wa bei nafuu ni wa korongo la Stiegler ambao ulikuwa katika mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya umeme katika mwaka 2012.
Mradi huo gharama kamili ya kujenga ni dola za Marekani bilioni 2.4 na mapitio ya taarifa yanaonesha kuwa mradi huu ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,100.
Mpango mkakati wa sekta ya umeme huo unaonesha kwamba mradi unatakiwa kujengwa kwa awamu tatu. Katika awamu ya kwanza Stieger I megawati 300 ungekamilika 2024, ya pili megawati 600 na ungekamilika 2026 na awamu ya tatu megawati 300 ungekamilika 2028.
Alisema mradi huo ulipangwa kuendeshwa na Mamlaka ya Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), lakini katika mapitio ya taarifa wamebaini kwamba, mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hivyo haiwezi kuendeleza mradi huo.

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link