NEW UPDATES

MAWASILIANO TATIZO MATIBABU YA LISSU PESA ZA BUNGE ZATUA NAIROBI.

MAWASILIANO TATIZO MATIBABU YA LISSU, PESA ZA BUNGE ZATUA NAIROBI

Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi wametofautiana kuhusu mvutano kati ya Ofisi ya Bunge na Chadema kuhusu fedha Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge kwa ajili ya matibabu wa Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Juzi, akizungumza na wanahabari kuhusu matibabu ya mbunge huyo wa Singida Mashariki, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema chama hicho kimepokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wananchi kwa ajili ya gharama za mbunge wa huyo ambazo zaidi ya Sh200 milioni zikiwamo zilizochangwa na wabunge ambazo hata hivyo, alisema Ofisi ya Bunge haijaziwasilisha.

Hata hivyo saa chache baada ya kauli hiyo ya Mbowe, Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema fedha hizo zimetumwa tangu Septemba 20 kupitia Benki ya Barclays, Tawi la Hurlringham, Akaunti Namba 0451155318 yenye jina Kenya Hospital Assocition.

Baadhi ya wasomi waliotakiwa kutoa maoni yaoi kuhusu suala hilo walikuwa na mitazamo tofauti. Mmoja alisema hali hiyo imetokana na kutokuwa na mawasiliano mazuri katika ya Serikali, Bunge na Chadema kuhusu matibabu ya Lissu na mwingine akisema kuna utaratibu wa kutuma fedha nje ya nchi hasa zinazotoka taasisi kubwa ikiwamo Bunge.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema Chadema inadai kuwa ndiyo inayosimamia matibabu ya Lissu wakati Serikali katika maelezo yake inaitaja familia ya Lissu na siyo chama hicho kwenye suala la matibabu yake.

“Mawasiliano kati ya taasisi hizi lazima yafanyike endapo Serikali na Bunge wakitambua anayemuuguza Lissu, hakuwezi kuwa na mvutano kama huu. Ndiyo maana Chadema ilishindwa kuliambia Bunge kwa nini wamechelewesha fedha za michango ya kiongozi wao,” alisema Mbunda.

Mbunda alisema hali ya kutokuwa na mawasiliano kati ya Serikali, Bunge na Chadema imesababisha kila mtu kutoa taarifa kwa umma juu ya kinachoendelea katika matibabu ya Lissu badala ya kuyamaliza ndani kwa ndani.

“Hatua hii ya kutoka hadharani inalenga kila upande kutafuta huruma kwa Watanzania dhidi ya matibabu ya Lissu jambo ambalo si jema na halijengi kwa sasa badala ya kujikita kwenye matibabu ambayo ni kipaumbele ili afya ya mbunge huyo izidi kuimarika,” alisema. Mhadhari wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Salim Hamad hakuwa mbali na Dk Mbunda. Alisema kinachooneka kwa sasa pande hizo kujisafisha na kutaka huruma kwa wananchi.

“Hapa kuna pande mbili, upande wa kwanza unasema hauna imani dhidi ya mwenzake na unasema haujafanya kitu katika sakata hili. Lakini kila upande unataka kuonyesha kwamba umeshiriki kikamilifu katika mchakato huu wa matibabu ya Lissu,” alisema Hamad.

Alisema jambo hilo halisaidii kwa sasa badala yake wajikite katika matibabu ya mbunge huyo. Pia alisema kinachohitaji hivi sasa ni Bunge kuweka kanuni zitakazotumika pindi linapotokea suala la dharura kama la Lissu.

Alisema licha ya Bunge kujiwekea utaratibu maalumu wa matatibu kwa wabunge wao pindi wanapopata matatizo mbalimbali ikiwamo ugonjwa, lakini ni wakati mwafaka kuweka kanuni itakayoainisha mchakato mzima wa ni wapi atakwenda kutibiwa na gharama zake pindi inapotokea dharura ili kuondoa sintofahamu kama ilivyojitokeza.

“Binadamu hujifunza kutokana na mifano na hili siyo kosa. Hili la Lissu ni mfano kwa hiyo ni vyema njia mbadala zichukuliwe kwa siku za baadaye kwa sababu pia ni viongozi wa kitaifa. Suala hili likiachwa halitaleta picha nzuri, imeshaonekana upande mmoja hauna imani na mwingine ndiyo maana walitaka mgonjwa wao akatibiwe nje ya nchi,” alisema Hamad.

Hata hivyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, George Shumbusho alikuwa tofauti na wasomi wenzake hao akisema hakuna tatizo lolote kama fedha zimeshatumwa labda Mbowe aibuke tena na kusema bado hazijatumwa.

“Zimechelewa wapi na kwa nini zimechelewa, hii si ya kazi Bunge. Lakini jana watu wengi waliotembelea mitandao ya kijamii watakuwa mashahidi baada ya Bunge kutoa taarifa ile,” alisema Profesa Shumbusho.

Imeandikwa na Bakari Kiango(Dar) na Mussa Juma (Nairobi)

Share :

Facebook Google+ Twitter

Related Posts :

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link