Kilio kipya CHADEMA, Diwani mstaafu aliyevamowa Afariki Dunia
KILIO KIPYA CHADEMA, DIWANI MSTAAFU ALIYEVAMIWA AFARIKI DUNIA
Wakati tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu likiwa halijapatiwa ufumbuzi juu ya akina nani waliohusika, chama hicho kimepaza sauti kikitaka tukio la kuvamia na kuuawa kada wake lichunguzwe haraka.
Kada huyo, diwani mstaafu wa Kata ya Ngoma wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Clezensia Mihado (55) alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuvamiwa nyumbani usiku wa manane.
Katika uvamizi huo, Clezensia alijeruhiwa kichwani na kitu chenye ncha kali Septemba 19, baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumbani kwake akiwa amelala na mumewe, Peter Bandama (62).
Katibu wa Chadema Wilaya ya Ukerewe, Deonatus Makalanga alisema matukio ya uvamizi yamekuwa na mwendelezo, vinaashiria uvunjifu wa amani.
Makalanga alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha waliohusika na tukio hilo wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.
Alisema matukio ya uvamizi yanayolenga kuchukua uhai wa wananchi yamekuwa yakiripotiwa kila mara, lakini hawaoni hatua mathubuti zinazochukuliwa na Serikali kuyakomesha.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nantare, Mkama Bandoma alisema tukio la uvamizi katika makazi ya diwani huyo lililoambatana na kuvunja milango na kujeruhi limeibua hofu kijijini hapo.
Akizungumza na gazeti hili jijini Mwanza jana, mume wa marehemu, Bandama alisema mkewe alifariki dunia saa nne asubuhi juzi.
“Nimehangaika na mke wangu nikidhani atapona, hali yake itaimarika, lakini imeshindikana. Hata sijui nieleze nini labda akili yangu ikitulia nitapata ufumbuzi lakini kwa sasa haipo sawa,” alisema. Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kuelekea Kijiji cha Nantare wilayani Ukerewe kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika leo.
Share :
No comments
https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link