NEW UPDATES

BREAKING: WAZIRI SIMBACHAWENE AJIUZULU KWA AGIZO LA RAIS MAGUFULI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.

Waziri Simbachawene ameandika barua hiyo muda mfupi tu tangu Rais Magufuli alipowataka viongozi wote aliowateua na wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.

Mbali na Simbachawene, wengine waliokuwa wametakiwa kukaa pembeni ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani ambaye alituhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lenye dhamana ya kusimamia madini.

Mbali na Ngonyani, mwingine ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi naye amepaswa kupisha uchunguzi ambao Rais ameagiza ufanywe na vyombo vya ulinzi na usalama haraka iwezekanavyo.

Rais Dkt Magufuli ametoa maagizo hayo leo alipokuwa akipokea ripoti hiyo ya uchunguzi wa madini kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye aliipokea jana kutoka katika kamati zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akiyasema hayo, Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi kwa wateule wake waliotajwa tajwa katika ripoti hizo lakini akasema kuwa, uchunguzi hauwezi kufanyika wakati kiongozi akiwa bado yupo serikali. Baada ya kusema hivyo, Rais Magufuli alisema anaamini kuwa viongozi hao watakaa pembeni kupisha uchunguzi.

Hafla hiyo ya kukabidhi ripoti ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai, Wenyeviti wa kamati mbili za Tanzanite na Almasi, Dotto Biteko na Mussa Azzan Zungu ambao wote ni wabunge.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa jumuiya ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na viongozi waandamizi wa serikali.

Rais Magufuli ameendelea kuwasisitiza watanzania kuwa wazalendo kwani rasilimali za nchini za nchi zinaibiwa na watanzania wanazidi kubaki katika umasikini uliokithiri.

Baada ya kuhutubia, Rais Magufuli alikabidhia nakala za ripoti hiyo kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili vianze kufanya kazi mara moja na sio kuendelea kukaa huku mali za watanzania zikiibiwa.

Share :

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link