NEW UPDATES

MAJIJI 9 MAZURI YA KUISHI BARANI AFRIKA.


Pamoja na imani mbaya walizonazo watu wa mabara mengine kwamba Afrika ni uwanja wa vita, ukame na umaskini wa kutupwa, itawashangaza sana kujua kwamba bara hili lina miji mizuri yenye viwango bora vya maisha sawa na miji mingine duniani. Barani Afrika kuna majiji yaliyoendelea na yenye mchanganyiko mkubwa wa watu wa maeneo mbalimbali kama yalivyo majiji mengine duniani, barabara nzuri, umeme, huduma nyingine za kijamii pamoja na fursa za kujiendeleza kiuchumi – mambo ambayo huwavutia watu wengi kuanzisha masiha sehemu fulani.

Yafuatayo ni majiji kumi barani Afrika ambayo mtu kutoka nchi yoyote anaweza kuishi vizuri bila gharama kubwa za masiha:

Cape Town, Afrika Kusini

Cape Town ni moja ya majiji mazuri sana ulimwenguni na lina starehe pamoja na anasa nyingi sana –  linapatikana katikati ya Bahari ya Hindi na milima. Upatikanaji wa nyumba za kuishi unatofautiana. Jiji hili lina sehemu nyingi kwa ajili ya utalii wa kupanda milima na michezo ya kwenye maji, pia kuna viwanda takribani 100 vya mvinyo vinavyotengenezwa baadhi ya bidhaa bora zaidi duniani za mvinyo. Cape Town ni kituo cha sekta za bima na teknolojia ya digitali barani Afrika. Utoaji wa usafiri wa umma jijini umefanyiwa maboresho makubwa na kulifanya kuwa miongoni mwa majiji ambayo ni bora kuwa na gari lako binafsi.

Accra, Ghana

Accra ni jiji linalowafaa wenye mitoko mingi ya mwisho wa wiki hasa kwa wasafiri na watalii wa hali ya juu hasa kwa migahawa ya kifahari, starehe za usiku na maduka makubwa ya kimataifa. Kuna maeneo mengi wanayoishi watu wenye maisha ya juu kama East Legon, sehemu ya watu mashuhuri – Accra Mall—na Osu, ambao wengi wanaujua kwa jina la Mtaa wa Oxford “Oxford Street” kwa kuwa na idadi kubwa ya maduka ya kifahari. Ukarimu wa watu wa Ghana ni miongoni mwa mambo yanayowavutia wageni wengi kutaka kutembelea na kuishi jijini Accra. Hali ya hewa ya kitropiki hufanya papendwe zaidi na wageni. Kipaumbele cha serikali ya nchi hiyo kutengeneza miundombinu ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia fedha wanazopata kutoka kwenye makampuni ya kigeni yaliyowekeza nchini humo, ni rahisi kutabiri kwamba Accra litakuwa jiji zuri zaidi ya lilivyo sasa baada ya miaka kadhaa.

Nairobi, Kenya

Nairobi limekuwa ni jiji la Afrika linalopendwa zaidi na makampuni mengi ya kimataifa yanayotaka kuwa na matawi barani Afrika. Nairobi ni jiji lenye aina ya maisha kama yaliyo kwenye majiji yote duniani; Nairobi ni jiji lenye huduma bora za sekta ya teknolojia na linasifika kwa kuwa na huduma bora zaidi za mtandao wa Intaneti barani Afrika. Kuhusu makazi, kuna nyumba nyingi karibu na mijini kwa gharama nafuu ikilinganishwa na majiji mengi barani Afrika pamoja na majumba ya kifahari yenye mabwawa ya kuogelea na kumbi za mazoezi.

Ingawa kutembea kwa miguu kulijua jiji hilo yawezekana ikawa ni kazi ngumu, machaguo mengine yenye gharama za kawaida ni pamoja na usafiri wa mabasi aina ya matatu na baiskeli za boda-boda zinazotumiwa sana na wenyeji. Katika miaka ya hivi karibuni, makampuni na taasisi nyingi za kimataifa zimekuwa zikifungua matawi yake jijini Nairobi, kama Taasisi ya Rockefeller, kampuni ya General Electric na Shirika la Utangazaji la China (CCTV).

Johannesburg, Afrika Kusini

Tangu unashuka kutoka katika ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo (ORTIA), utaona wazi kwanini Johannesburg linasemwa kuwa ni jiji lenye hadhi ya kimataifa. Uwanja huu wa ndege ni moja ya viwanja bora kabisa duniani. Johannesburg pia ni moja ya majiji ya kisasa zaidi barani Afrika lenye fursa nyingi za uwekezaji na ajira. Miaka michache iliyopita, serikali ya Afrika Kusini iliwekeza kuliboresha jiji hilo na sasa mitaa ya jiji hilo ni misafi zaidi na majengo yamefanyiwa ukarabati mkubwa.

Jiji hili pia lina maduka makubwa (malls) yenye hadhi ya kimataifa kama vile Sandton City na Eastgate. Kama utahitaji hewa ya asili, jiji la Johannesburg ina sifa ya kuwa na msitu mkubwa zaidi duniani uliopandwa (si wa asili). Jiji hili la Joburg, kama linavyojulikana kwa wengi, lina maduka na migahawa mingi, na limepewa jina la utani la “Kitovu cha shughuli za uchumi Africa”.

Gaborone, Botswana 

Mji huu Mkuu wa Botswana una utulivu wa kisiasa na wenye uchumi imara juu ya sifa ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa zaidi wa madini ya almasi duniani. Jiji hili linasemwa kuwa ni miongoni mwa majiji yenye utulivu zaidi barani Afrika. Bila kujali udogo wake (likiwa na watu 230,000), jiji la Gaborone mchanganyiko mkubwa wa watu na lina maeneo mengi ya kitalii. Umaarufu wa jiji la Gaborone mpaka kuingia kwenye orodha ya majiji mazuri zaidi ya kuishi barani Afrika yawezekana ikahusushwa pia na ukuaji wake wa haraka wa sekta ya utalii, inayovutia watalii wengi kutembelea nchi hiyo kila mwaka. Gabs, kama linavyojulikana kwa kifupi na watu wengi, sasa linaashiria madini ya almasi – yanayochimbwa kwa wingi sana na kuchochewa ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Tunis, Tunisia

Mambo mengi sana yamebadilika toka kuanza kwa machafuko takriban miaka miwili iliyopita. Tunisia yawezekana ikawa ni moja ya nchi ndogo zaidi Kaskazini mwa Afrika, lakini kwa sasa inaendelea kwa kasi sana. Jiji la Tunis lina uhusiano wa karibu na Ufaransa, lakini lina muingiliano mkubwa sana wa watu wa tamaduni tofauti. Ni moja ya miji ya kwanza ya Kiarabu ambayo pia ni sehemu ya urithi wa dunia inayotambuliwa na taasisi ya UNESCO. Kiwango cha makadirio ya maisha kwa wananchi wa kawaida wa jiji hili ni kikubwa sana (miaka 74.6). Moja ya sababu yawezekana kuwa jiji la Tunis lilitajwa kuwa nafasi ya pili katika majiji ambayo wakazi wake wana furaha zaidi barani Afrika. Likiwa limeshawahi kuwa jiji tajiri zaidi duniani kwa nchi za Kiislamu, jiji hili linasemwa kuwa ni miongoni mwa majiji yenye gharama nafuu zaidi za maisha (hasa kwa wageni) ikilinganishwa na majiji mengine barani humu. Kujua sehemu mbalimbali za jiji la Tunis ni rahisi kwakuwa kuna mtandao mzuri wa reli ambao unaunganisha jiji hilo na sehemu nyingine za nchi.

Dar es Salaam, Tanzania 

Dar es Salaam ni jiji ambalo kila mwaka idadi ya wakazi katika jiji hilo huongezeka kwa asilimia 3 na kulifanya kuwa jiji namba tatu kwa ukuaji wa haraka zaidi barani Afrika. Jiji hili ndio kitovu cha siasa na uchumi wa nchi ya Tanzania na kwa miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa uwekezaji mkubwa ukifanyika katika sekta ya elimu. Mabilioni ya shilingi yametumika katika kipindi cha miaka sita iliyopita ili kuboresha barabara za jiji hilo na kufanya usafiri wa umma uwe ni rahisi zaidi na wenye uhakika. Likiwa ni karibu sana na ukanda wa ikweta, jiji hili linakuwa na hali ya hewa ya ukanda wa kitropiki muda mwingi wa mwaka – hali ambayo huvutiwa watalii wengi sana. Kimefanyika uwekezaji mkubwa kwenye elimu, zikiwemo juhudi za makusudi za kutoa elimu ya bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika shule zinazomilikiwa na serikali, juhudi zilizopongezwa sana na kuungwa mkono na taasisi za kimataifa hasa baada ya idadi ya wanafunzi wapya walioandikishwa shule ya msingi ilipofika zaidi ya asilimia 90 ya matarajio. Kwenye jiji hili pia ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, chuo kikuu cha kwanza kabisa cha umma nchini Tanzania ambacho kina zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kimeongeza idadi ya wanafunzi wanaopokelewa chuoni hapo.

Windhoek, Namibia

Kuanzia lugha mpaka majengo, utamaduni wa Ujerumani umeliathiri sana jiji la Windhoek; lina huduma nzuri za afya na shule pamoja na taasisi za elimu. Windhoek ni jiji dogo lakini kila taasisi ya Serikali inapatikana hapo na kulifanya kuwa kitovu cha shughuli za siasa, utamadunikijamii na kiuchumi nchini Namibia. Kama nchi ya Namibia inajulikana zaidi kwa kuwa na Jangwa la Namib, Jangwa la mwanzo kabisa kuwahi kutokea duniani, basi jiji la Windhoek linajulikana zaidi kwa bia yake. Windhoek Lager ni moja ya bia zinazonywewa na watu wengi zaidi kwakuwa inauzwa kwenye nchi zaidi ya 20, Windhoek ni jiji hili lenye baa nyingi. Unapotembea kwenye mitaa ya jiji la Windhoek, tarajia kukutana na watu wengi toka maeneo tofauti, kuanzia wenyeji wa makabila ya San, Hereo, na Kavango mpaka wataalamu toka nchi mbalimbali za Ulaya. Jiji la Windhoek linavutia sana kwa sababu ya usafi wake, salama na wepesi wa kutembea maeneo ya jiji hilo kwakuwa kuna barabara nzuri sana.

Kigali, Rwanda

Jiji hili la Kigali lililopo katikati ya Rwanda ni jiji lenye wakazi takriban milioni moja, wengi wao wakiwa ni wageni toka nchi mbalimbali. Jengo jipya la ghorofa 20 linalojulikana kama “Kigali Tower,” ni jengo la ofisi na maduka lililochangamsha sana jiji hilo. Ujenzi wa barabara mpya uliokamilika hivi karibuni umesaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara za jijini humo na kulifanya kuwa moja ya majiji yanaendelea kwa kasi sana barani Afrika.

Utalii unabaki kuwa chanzo muhimu cha mapato kwakuwa ni sekta inayoliingizia Taifa hilo fedha nyingi za kigeni: Uboreshwaji wa jiji hili bila shaka utaongeza uwekezaji mkubwa katika sekta za hoteli, huduma na utalii. Hali ya hewa ya jiji hili ni ya kawaida muda mwingi na kuna shughuli kadhaa za kuvutia na matukio ya kijamii yanayofanywa na wazawa wa nchi hiyo. Watu ni marafiki na muda wote ni wakarimu wa wageni.

Majiji mengine ambayo bila shaka yalistahili kuwepo kwenye orodha hii ni pamoja na jiji la Kumasi nchini Ghana ambalo watu wake wamewahi kutajwa kama watu “marafiki” zaidi kwa wageni ikilinganishwa na bara zima, jiji la Algiers ambalo ni Mji Mkuu wa Algeria linalojulikana sana kwa mchanganyiko wa tamaduni za Waarabu na Wafaransa, fukwe nzuri, idadi kubwa ya wageni pamoja na uchumi wa juu sana.

Share :

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link