NEW UPDATES

CHUO KIKUU HATARINI KUPIGWA MNADA NA BENKI


Na  MatukiodaimaBlog 

KATIKA  harakati  za  kukinusuru  Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira  Tawi la  Mbeya kisipigwe  mnada  na Benki  ya Biashara ya  Afrika (CBA) Askofu  Mstaafu  wa Kanisa la  Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya  Iringa ambae  pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho,   Dkt  Owdenburg Moses Mdegela amesema  ameamua  kujilipua kunusuru  chuo  hicho  kwa  kuanza  kutembeza  bakuri kwa  waumini  wote wa KKKT  nchini  wakiwemo viongozi  na  wanasiasa  ambao ni  walutheri kama  mke wa Rais wa awamu ya  tatu mama Anna Mkapa   na  wengine

Dkt  Mdegella  amesema  amechukua  hatua  hiyo  ya  kujilipua  baada ya  kuona  dalili   ya  chuo  hicho  kupigwa  mnada akizungumza  na  wanahabari  juu ya hatua  hiyo  aliyochukua Dkt. Mdegela a alisema chuo hicho ambacho ni sehemu ya kanisa hilo kipo katika hatari ya kuzama kwa kushitakiwa na kuuziwa  mali zake, na kuitia aibu KKKT kama uvumilivu wa benki hiyo  utafika mwisho kwa kushindwa kulipa deni hilo.

Alisema ameamua kujilipua na kuomba msaada huo kupitia vyombo vya habari baada ya kuona jitihada na mikutano mingi ya kulipa deni na malimbikizo yake ya riba kwa kupitia taratibu za kawaida za kanisa yakipata vikwazo kila wanapokutana kujadili.

Alisema Desemba, 2013 chuo hicho kilikopa kutoka katika benki hiyo zaidi ya Sh Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na madarasa ya chuo mkopo ambao sehemu yake haukutumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Bila kutaja majina ya wahusika wa matumizi mabaya ya fedha za mkopo huo, Dk Mdegela alisema baadhi ya wajumbe wa bodi na viongozi wa chuo hicho wanapaswa kubeba lawama na kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na ubadhirifu uliofanywa.

“Tumefanya ukaguzi wa hesabu za mkopo huo mara mbili. KKKT ilifanya ukaguzi wake lakini pia kulikuwa na mkaguzi wa nje. Kwa pamoja wamebaini kuwepo kwa  ubadhirifu mkubwa, rushwa na ufisadi” alisema.

Alisema ukaguzi wa awali unaonesha asilimia 45 ya mkopo huo ndiyo iliyotumika kwa kazi iliyokusudiwa huku asilimia 55 iliyobaki ikitumika kwa malengo tofauti na ujenzi uliokusudiwa.

“Suala hili limeshakabidhiwa Polisi na kwa wanasheria ili hatua za kisheria kwa wahusika zichukuliwe. Na kwa taarifa ni kwamba wahusika wanaotuhumiwa  kwa ubadhirifu huo wamekwisha simamishwa kazi,” alisema bila kuwataja wahusika hao.

Dk Mdegela ambaye pia ni mwenyekiti wa timu ya maaskofu watatu wa kunusuru chuo hicho (Dk Mdegela, Dk. Alex Malasula na Dk Abednego Mshahara)  alisema kwa makubaliano ya kulimaliza suala hilo kiungwana, benki hiyo imewataka kulipa Sh Milioni 275 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu na kwamba marejesho ya deni hilo yataendelea kufanywa kila mwezi.

“Mahali lilipofika suala hili sio mahali pa  kunyamaza, tunataka kila mlutheri na sharika zake zote nchini zijue kinachoendelea na wachangie kunusuru chuo hicho ili kuliondolea kanisa aibu,” alisema.

Alisema ili kufikia makusanyo hayo kutakuwa na makundi manne, la kwanza litajumuisha watu watakaombwa kuchangia Sh 100,000 na kuendelea, la pili watachangia kati ya Sh 50,000 na Sh 100,000, la tatu kati ya Sh 20,000 na Sh 50,000 na la nne kiasi chochote chini ya Sh 20,000.

Pamoja na mapendekezo hayo alisema, watu wataruhusiwa kuchanga zaidi ya kiwango kinachopendekezwa katika makundi yao kwa kadri watakavyoguswa na jambo hilo alilosema ni tatizo kwa kanisa.

“Lakini pia nitalazimika kukutana na walutheri maarufu ambao ni waajiriwa katika taasisi mbalimbali, wafanyabishara na wanasiasa na wadau wengine wa KKKT nchini,” alisema na kuwataja baadhi yao kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei.

Pamoja na kupitisha kapu hilo, alisema wanaendelea kuandaa njia nyingine zitakazosaidia kufikia lengo la makusanyo na marejesho ya deni hilo hadi litakapokwisha.

Dk Mdegella aliwataka wadau hao kuchangia chuo hicho kupitia akaunti maalumu No 108433100028 iliyofunguliwa katika benki hiyo ya CBA kwa ajili ya kukusanya na kulipa deni hilo.

Alisema yote hayo anayafanya kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa, Askofu Dk Frederick Shoo na kwa niaba ya Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Bodi ya Wadhamini ya Chuo, Baraza la Uongozi na Maaskofu wenzake na wajumbe waliopewa kazi ya kunusuru chuo hicho.

Kwa yoyote anayehitaji ufafanuzi zaidi anaweza kuwasiliana jinsi ya kukisaidia chuo hicho kupitia simu namba 0754313173,” alisema.

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link