WAZIRI KAIRUKI ATANGAZA NEEMA KWA WATUMISHI WALIOKUTWA NA VYETI FEKI
WAZIRI KAIRUKI ATANGAZA NEEMA KWA WATUMISHI WALIOKUTWA NA VYETI FEKI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, leo Bungeni amesema kuwa wizara yake imetoa muda wa kukata rufaa kwa watumishi wote wa umma waliotajwa katika tuhuma ya kughushi vyeti.
Waziri Kairuki aliyasema hayo bungeni Dodoma leo, na kueleza kuwa kama kuna yeyote anayeona kuwa ameonewa basi anaweza kukata rufaa na vyeti vyake kuhakikiwa upya.
Angella Kairuki alisema kuwa watumishi wote watakaokata rufaa kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, wapeleke kwa waajiri wao vyeti vile vile ambavyo viko katika majalada yao ya utumishi, huku nakala zikipelekwa Baraza la Mitihani (NECTA).
“Wanaotaka kukata rufaa kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, nakala iende Baraza la mitihani na ipitishwe kwa muajiri wao, na iambatanishe vyeti vile vile ambavyo viko katika jalada lake binafsi la utumishi na ambavyo vilihakikiwa kwa mara ya kwanza. Mwajiri akishavipitisha atavipeleka moja kwa moja baraza la mitihani halafu seti hiyo nyingine itapelekwa kwa Katibu mkuu utumishi,” alisema Waziri.
Aidha amewaonya wale wote ambao wanataka kutumia mwanya huo ili kudanganya kwa mara nyingine, yaani kupeleka vyeti vyao ili vihakikiwe upya huku wakijua kwamba ni kweli walighushi, kuwa watakapobainika adhabu yao itakuwa kubwa zaidi ya hii iliyotolewa awali.
“Tutavipitia kwa kina kuliko hata awali. Kwa hiyo niombe tu kutoa angalizo, tusifanye nalo mzaha kwa wale ambao wanatusikiliza. Tunatoa ruksa hiyo ya rufani, lakini kweli iwe mtu ana uhakika kuwa ameonewa. Kwa sababu itakapotokea mtu ametumia fursa hii ya rufani na anaujua ukweli, na matokeo yakarudi vile vile, kwa kweli adhabu itakuwa kali zaidi,” alisema Waziri Kairuki.
No comments
https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link