NEW UPDATES

MAJINA YA WACHEZAJI 5 WANAOGOMBEA TUZO YA MCHEZAJI BORA TANZANIA

Michezo

Wachezaji watano wameteuliwa (nominees) kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2016/2017.

Walioteuliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni Aishi Manula (Azam FC), Haruna Niyonzima (Yanga), Mohamed Hussein (Simba), Shiza Kichuya (Simba) na Simon Msuva (Yanga).

Majina hayo yatapigiwa kura na makocha, makocha wasaidizi na manahodha wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na wahariri wa michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Wahusika watatumiwa fomu maalum za kupiga kura kwenye email za klabu zao na vyombo husika vya habari. Mwisho wa kupiga kura ni saa 6 usiku ya Jumanne, Mei 23 mwaka huu.

Hafla ya kutoa tuzo hiyo ambayo inaratibiwa na Kamati ya Ushauri ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itafanyika Mei 24 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

MU-IVORY COAST KUCHEZESHA TANZANIA, ANGOLA

Abou Coulibaly atachezesha mchezo wa pili wa Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Serengeti Boys ya Tanzania na Angola utakaofanyika Uwanja wa l’Amitie kuanzia saa 11.30 jioni kwa saa za Tanzania.

Mwamuzi Coulibaly atasaidiwa na Mamady Tere wa Guinea na Attia Amsaad wa Libya wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Mohamed Maarouf wa Misri huku Kamishna akiwa ni Ismael Locate wa Reunion.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Nyundo Shime amesema kwamba ameiona Angola ikicheza na Niger katika mchezo wa kwanza uliofanyika mara baada ya mchezo wa Serengeti na Mali.

“Utakuwa ni mchezo wa ushindani. Nasi tunakwenda kushindana. Matokeo ya awali ya sare kwa timu zote mbili yanafanya mchezo huu kuwa mgumu kwa kundi B.

“Angola ni wa kuchungwa sana. Kwa sababu walipocheza na Niger waliweza kusawazisha mabao mawili kipindi cha pili. Hii inaonesha kuwa ni wepesi wa kusoma makosa yao na kujirekebisha.

“Ila kikosi changu kiko imara, nikiamini kwamba kesho nitapata matokeo mazuri. Watanzania waendelee kutuombea. Tutafanikiwa,” amesema Shime maarufu kwa jina la Mchawi Mweusi.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments

https://instagram.com/bakihotnews?utm_medium=copy_link